
“Kabla ya kuanza mechi, kocha unatakiwa kumchukua mchezaji mmoja mmoja na kumzungusha eneo zima la uwanja kwa dakika 30, tunafanya hivyo ili kumjengea mchezaji hali ya kuzoea mazingira ya uwanja kabla ya kucheza,” anasema kocha wa mpira wa kengele, Hashiru Tembo
Anasema wachezaji hupelekwa kila sehemu ya uwanja
utakaotumika kwenye mechi hiyo, ambazo ni kwenye goli wanalotakiwa
kufunga na kwenye goli lao kwa ajili ya kuzuia na mwisho wa uwanja, pia
katikati ili kung’amua urefu na ukubwa wa uwanja watakaoutumia.
Mpira wa kengele au ‘Goal ball’ ni mchezo
ulioanzishwa na raia wa Australia, Hanzi Lorenzen na raia wa Ujerumani,
Sepp Reindle mwaka 1946 kwa ajili ya kuwasaidia askari waliopigana vita
ya pili ya dunia na kupata matatizo ya macho.
Kwa mara ya kwanza nchini mchezo huu umechezwa
kwenye mashindano ya 20 ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za
Msingi Tanzania (Umitashumta) ya msimu huu kwenye viwanja vya Shirika la
Elimu Kibaha, Pwani.


Mpira wa kengele unavyochezwa
Hashiru Tembo ambaye ni kocha wa mchezo huo
anasema mpira wa kengele unachezwa na wachezaji wasioona (vipofu) na
wenye uoni hafifu ambao kabla ya kuanza kwa mechi wote huvaa vitambaa
vyeusi kuziba macho kwa ajili ya kuzuia wale wenye uoni hafifu kutoona
kabisa ili kuendana na wenzao (vipofu).
Timu nzima ina wachezaji wangapi?
Tembo anasema kila timu inasajili wachezaji wanne,
ambao kati yao watatu wanakuwa kwenye kikosi cha kwanza na mmoja
anakuwa mchezaji wa akiba, wanaoanza mmoja anakuwa mchezaji wa kati na
wachezaji wawili wa pembeni.
“Mchezaji wa kati mara nyingi anakuwa yule mwenye
hisia za haraka za kubaini mpira pale unapokuwa umerushwa golini kwao na
anapoudaka hatakiwi kuugusa zaidi ya mara mbili, akishagusa mara mbili
anapaswa kumpa mchezaji wa pembeni akigusa mara ya tatu hiyo ni faulo,”
anasema Tembo.
Anasema mchezaji wa kati ambaye ni muhimu kwa
ulinzi anapougusa mpira kwa kuwa ni mchezo wa wasioona, anapaswa kufanya
ishara ya kugusa mpira kwa nguvu kidogo ili kengele itoe sauti
kumwashiria yule wa pembeni kuwa anampa pasi.
“Akiugusa mara ya tatu hiyo ni faulo, na faulo za
mpira wa kengele ni kupigwa kwa penati, wakati wa upigaji wa penati
wachezaji wa pembeni wanapaswa kutolewa na kubaki yule wa kati peke
yake,” anasema Tembo.


Anasema mpira wa kengele hauna kona wala mpira wa
kurusha, goli linapofungwa timu iliyofungwa ndiyo inaanzisha mpira
kutoka pembeni mwa goli lao na mchezaji atakayetoa nje mpira unapelekwa
kuanzwa kwenye lango la timu pinzani.
No comments:
Post a Comment