Wednesday, July 30, 2014

MAPYA YAIBUKA KUHUSU SAKATA LA KUTUPWA VIUNGO VYA BINADAMU

SAKATA  la kutupwa kwa viungo vya binadamu  lililofanywa na Chuo Kikuu cha Tiba cha Kimataifa cha IMTU kilichopo Mbezi jijini Dar,  linadaiwa kuikumba Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) baada ya tanuru linalotumika kuteketeza viungo vya binadamu kuharibika kwa miezi sita sasa.
 

Fuvu la kichwa cha binadamu.
Uchunguzi uliofanywa na timu ya Uwazi kwa muda wa siku kadhaa ndani  ya hospitali hiyo, umebaini kuwa tanuru la Muhimbili ambalo lilikuwa na uwezo wa  kuchukuwa kilo 200 za uchafu kwa wakati mmoja vikiwemo viungo vya binadamu ili kuteketezwa linadaiwa kuwa ni bovu kama la IMTU.
Uchunguzi ukazidi kubaini kuwa baada ya mtambo huo kuharibika, uongozi wa hospitali hiyo uliamua kununua mashine nyingine Aprili, mwaka huu lakini hadi sasa haijafungwa.
Baadhi ya watumishi wa hospitali hiyo waliozungumza na waandishi wa Uwazi kwa nyakati tofauti kwa masharti ya kutoandikwa majina yao, walisema kukosekana kwa mashine hiyo katika taasisi hiyo nyeti kwa muda wa miezi sita ni aibu na hatari ndiyo maana baadhi ya watu wanadai kuwa huenda nao wanatupa viungo vya binadamu porini.
Kutokana na madai hayo, waandishi wetu walimtafuta Afisa Uhusiano Mkuu wa Muhimbili, Amaniel Aligalesha na kumuuliza ambapo alikiri kuwa mashine hiyo ni mbovu tangu Februari, mwaka huu.
“Lakini Aprili tumenunua mashine mpya ambayo haijafungwa,” alisema Aligalesha.
Alipoulizwa kuhusu mabaki ya viungo vya binadamu kwa kipindi chote hicho wanatupa wapi, alijibu:
  “Swali hilo sasa liko chini ya Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam hivyo kawaulize wao watawapa majibu sahihi.”
 
Gari aina ya center likiwa limebeba mzigo mkubwa wa viungo hivyo.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar, Suleiman Kova alipoulizwa aliwashangaa Muhimbili kwa kumsukumia suala hilo yeye.“Mambo ya mitambo ya Muhimbili au wanapotupa mabaki polisi wawajibie nini? Ilipaswa wajibu swali hilo wao na siyo polisi,” alisema  kwa ukali Kamanda Kova.
Wandishi wetu walifanya uchunguzi pia katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (Moi), ikagundua kuwa mashine yao ya kuteketezea viungo vya binadamu na vitu vingine inafanya kazi.
Julai 22, mwaka huu, jeshi la polisi kanda maalum liliunda tume kuchunguza sakata la Hospitali ya IMTU ambayo inaongozwa na ACP Jafar Mohamed ambaye ni mkuu wa upelelezi wa kanda hiyo ili kupata ukweli wa tukio hilo.
Hivi karibuni viroba 85 vilivyokuwa na viungo vya binadamu viligunduliwa katika eneo la Bunju B, Mto Mpiji jijini Dar vikiwa vimetupwa na tayari watu nane kutoka IMTU wametiwa mbaroni wakihusishwa na tukio hilo.

No comments:

Post a Comment