
Wakati sakata la kuokotwa kwa viungo vya binadamu likiendelea kutikisa nchi, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), kimesema kuwa hutumia maiti 25 kwa kuwafundishia wanafunzi kila mwaka.
Pia chuo hicho hakijawahi kuagiza maiti kutoka nje
ya nchi na kwamba ni mtu mmoja tu aliyewahi kutaka maiti ya mtoto wake
itumike kufundishia.
Kauli hiyo ya MUHAS imekuja siku chache baada ya
Serikali kuamua kuifungia Hospitali ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba
na Teknolojia (IMTU), baada ya kubaini kasoro kadhaa katika utendaji
wake.
Juzi, Serikali ilifanya ukaguzi wa kushtukiza
IMTU, baada ya hospitali hiyo kukumbwa na kashfa ya utupaji wa mabaki ya
viungo vya binadamu katika Bonde la Mto Mpiji, jijini Dar es Salaam
mwanzoni mwa wiki iliyopita.
Hata hivyo, wakati Tume ya Watu 15 iliyoundwa na
Serikali kuchunguza suala hilo ikiendelea na kazi, Mkuu wa Kitengo cha
Anatomy MUHAS, Profesa David Ngassapa amebainisha kuwa chuo hicho
hutumia maiti 25 kwa mwaka.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake jana,
Ngassapa alisema kuwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza hutumia maiti 20,
huku madaktari wanaorudi chuoni hapo kwa ajili ya mazoezi wakitumia
maiti tano.
No comments:
Post a Comment